
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita amemteua Monsinyo Novatus Rugambwa tokea Tanzania, kuwa Balozi mpya kwenye visiwa vya Sao Tome na Prince na kumpandisha hadhi kuwa askofu mkuu. Kabla ya uteuzi wake, Monsinyo Rugambwa alikuwa ni katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na wakimbizi.
Askofu mkuu mteule Novatus Rugambwa alizaliwa kunako tarehe 8 oktoba, 1957, Jimbo Katoliki la Bukoba. Alipadirishwa tarehe 6 Julai, 1986, Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania. Tangu tarehe 1 Julai, 1991 alianza utumishi wake wa kiplomasia, kwa kuiwakilisha Vatican huko Congo, Pakistan, New Zeland na Indonesia.
Tarehe 28 Juni, 2007, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita akamteuwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa wahamiaji na wakimbizi.
Ni mtaalam wa lugha ya Kiswahili, Kiingereza, Kiitalia, Kifaransa, Kihispania, Kijerumani, bila kusahahu lugha yake ya asili ambayo ni Kihaya, maarufu sana kwa Kanda ya Ziwa Victoria.
Jumuiya ya Watanzania Rome inampongeza Monsinyo Rugambwa na kumtakia mafanikio mema.
No comments:
Post a Comment